Maswali yanayoulizwa mara kwa mara

Je, malengo ya Oxford Global Languages ni yepi?
Lengo la mradi huu kwa ujumla ni kukusanya makala ya lugha 100 na kuyaweka mtandaoni na kuyafanya yawafikie watumiaji na wasanidi kote ulimwenguni. Kutimiza haya, timu husika inapaswa kuunda makala ya lugha na kamusi yanayoweza kuhifadhiwa, kuunganishwa, na kufikiwa kupitia njia mbalimbali. Mradi wa OGL utawezesha utengenezaji wa vifaa na raslimali mpya za dijitali zitakazoimarisha na kusaidia lugha ambazo hazijawakilishwa kikamilifu kidijitali pamoja na lugha kuu za kimataifa. Mradi huu utapatia lugha zote uwepo hai, mahiri na unaokua kwenye mazingira ya kidijitali, na kusaidia kuzirekodi, ikiwa ni pamoja na lahaja  na sajili zake.


Je, huwa mnachagua vipi lugha za kuzindua?
OGL inanuia kuwa na angalau lugha 100 kwa ujumla na tunajua kwamba tutachukua miaka mingi kutimiza. Tulianza na lugha kumi tu zilizo tofauti sana kutoka maeneo mbalimbali, kila moja yao ikiwa na viwango tofauti vya uwepo wa kidijitali, ili tuonyeshe kanuni za OGL na kuimarisha mawazo yetu tunavyoendelea. Tunavyosonga mbele tutaendelea kujumuisha aina nyingi za lugha ikiwa ni pamoja na lugha za kimataifa na zile ambazo hazijawakilishwa kikamilifu kidijitali.


Je, ni lugha gani zilizojumuishwa kwenye mradi? Na ninaweza kupata wapi lugha zitakazozinduliwa?
Unaweza kufuatilia lugha ambazo tumeshazindua na ugundue ni lugha gani zinazoongezwa kwenye mradi hapa. Vinginevyo, unaweza kujiandikisha kwa kijarida chetu cha Oxford Global languages hapa.


Je, huwa mnafanya kazi na mashirika ya ndani na bodi za serikali kwenye mradi?
Ndiyo, lakini sisi si washirika rasmi wala si wanachama wa shirika lolote lililopo. Oxford Global Languages ni mradi mpya na huru kabisa unaosaidiwa na Oxford University Press, ambayo ni sehemu ya wito wa Chuo wa kueneza mafunzo na elimu kote ulimwenguni. Hata hivyo, tuko tayari kufanya kazi kwa ushirikiano na shirika lolote linalounga mkono au linalovutiwa na malengo ya OGL na, mradi unavyoendelea kukua, tutatafuta ushirikiano na bodi za kimataifa za lugha, wasomi, vyuo vikuu, na kampuni. Tumeshajenga mahusiano mazuri na washirika, wasomi, na wataalam wa lugha ulimwenguni. Ikiwa unataka kuwa kwenye mradi, tafadhali wasiliana nasi.


Je, makala hutoka wapi kwa kila tovuti ya lugha?
Makala yetu yanahusu lugha halisi, matumizi halisi, na watumiaji halisi. Kwa lugha zingine zilizoko kwenye mradi wa OGL hadi sasa kamusi zao hazipo. Kwa hivyo, ilhali kuna nyakati zingine ambazo huwa tunatumia kamusi iliyopo kuanzia, nyakati zingine huwa tunahitaji kuanza na kiunzi cha maana pamoja na raslimali ya matumizi ya lugha – yote yaliyoandikwa – ambapo huwa tunadondoa kiotomatiki aina zote za maelezo ya lugha. Hii husaidia wanaleksikografia kupata msingi wa kuanzia kuunda miseto mipya ya data. Pia, tunawaalika, enyi watumiaji wa lugha, mhusike, kwa mfano kwa kuchangia tafsiri na maelezo mengine yanayohusu lugha yenu. Tunaita michango hii ‘makala kutoka kwa watumiaji’, na yanatumiwa kufanikisha shughuli ya uhariri inayojenga zaidi makala yapatikanayo kwa kila lugha.

Je, ‘makala kutoka kwa watumizi’ hupotosha lugha ‘ya kawaida’?
Masuala ya lugha huzua mjadala kwa sababu watu wengi huwa na hisia nzito kuhusu lugha waizungumzayo. Baadhi ya watu huhisi kwamba ‘wataalam’ pekee ndio walio na ufahamu wa lugha na kwamba matumizi ya semi au maneno yasiyo rasmi ni ‘mbaya’ na hayafai kuwepo kwenye kamusi. Tunaamini kwamba mifano yote ya lugha, iwe rasmi au la, ni muhimu, na kuwa wazungumzaji asili wanajua mengi tayari kuhusu lugha yao yenyewe. Lengo letu na mradi wa OGL ni kukusanya maelezo mengi zaidi iwezekanavyo kuhusu jinsi ambavyo lugha inatumiwa – na watumiaji wake wote – ili tufanyayo yawe na manufaa kwa kila mtu.

Baadhi ya lugha zimeshughulikiwa zaidi kuliko zingine. Kwa nini?

Mojawapo ya kanuni za mradi huu ni kuanza na kidogo, kisha tukuze. Kwa hivyo, hata kama tuna kiasi kidogo cha makala yanayopatikana kwa lugha fulani, tunaweza kuyajumuisha kwenye mradi ili tuwaruhusu watumiaji waanze kutumia makala hayo na watupe maoni. Mradi unavyoendelea, ndivyo makala yanavyokua.

Je, ninawezaje kuongeza kamusi yangu au lugha yangu kwenye mradi wa OGL?
Bila shaka hatuwezi kujumuisha kila kitu, lakini kuna baadhi ya lugha ambazo hatuna makala yoyote yanayopatikana. Ikiwa wewe, chuo chako kikuu, au shirika lako lina chochote unachofikiri kwamba kinaweza kuvutia mradi huu, au mna mapendekezo kuhusu mwelekeo ambao OGL inapaswa kuchukua, tafadhali wasilianeni nasi.


Je, jukumu la Oxford katika kuendeleza lugha kutoka kote ulimwenguni ni gani?
OUP ni shirika la kimataifa lililo na raslimali, ujuzi na maarifa ya kipekee, na kama sehemu ya kazi yetu, tunanuia kushiriki raslimali hizi kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo. Huwa tunafanya kazi na wataalam wa lugha asili, ambao wapo katika jamii yao ya lugha, kuunda makala ya kipekee kwa lugha yao. Sehemu ya kazi yetu ni: kushiriki raslimali zetu kwa manufaa ya jamii yote kwa ujumla.


Je, jamii za lugha asili zinapaswa kushiriki kwa kiwango kipi?
Kushiriki kwa jamii ni muhimu. Tunataka jamii za lugha asili zishiriki kwenye mradi, iwe ni katika kupendekeza makala au kufikia tu raslimali zetu. Mradiunavyoendelea, ndivyo mipango mipya itakavyokuwepo itakayoruhusu jamii za lugha kujenga na kutumia makala katika lugha zao.


Je, ni nini kinachofanya OGL kuwa tofauti?
Mipango mingi hutoa tovuti za lugha zisizotoza malipo au hunuia kukusanya raslimali za lugha, lakini kuna mipango michache inayounda raslimali nyingi za kina za misamiati ya lugha nyingi, ikizingatia kanuni madhubuti za kileksikografia kama OGL inavyofanya. Makala yanatokana na matumizi halisi na yanasasishwa na kudumishwa kwa matumizi ya muda mrefu, inayofanya lugha kuwa hai na inayosisimua. Sababu ipo katika kazi yetu – tunajenga kwa minajili ya mustakabali wa kudumu wa lugha kote ulimwenguni, bali sio kwa manufaa ya muda mfupi.


Je, makala ya OGL ni ya bila malipo?
Tovuti zote za OGL zinatumika bila malipo. Unaweza kutafuta maneno, tafsiri, na maelezo mengine ya lugha. Tovuti hizi ziko katika lugha asilia na hata Kiingereza ili ziwe zinazoweza kutumika kikamilifu iwezekanavyo.

Pamoja na kuzindua lugha za OGL kama tovuti, tunazizindua pia kama sehemu ya mradi wa Kiolesura Programishi cha Matumizi yaani API. Ikiwa wewe ni msanidi anayetaka kutumia data ya lugha kwenye programu yako, unaweza kufikia makala ya OGL kwa matumizi ya kibinafsi na matumizi yaliyodhibitiwa bila malipo, na unaweza kujiandikisha kwa mipango yetu ya kila mwezi ikiwa ungependa kuendelea kutumia APIs hizo zaidi. Tafadhali tembelea ukurasa wetu wa API au wasiliana nasi hapa kwa maelezo zaidi.


Je, ni wapi ninapoweza kupata maelezo kuhusu  kushiriki katika mradi wa OGL?

Tungependa sana uwasiliane nasi, kwa hivyo wasiliana nasi ikiwa:

  • ungependa kujua mengi kuhusu mradi huu
  • unahisi kwamba wewe au shirika lako lingependa kushirikiana na Oxford Dictionaries katika kutusaidia kutimiza malengo ya OGL.
  • ungependa kuwasiliana nasi kwa kujiandikisha kwa kijarida cha OGL

Wasiliana nasi hapa.